Sheria ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009 inaweka mfumo wa kisheria na kitaasisi wa usimamizi na utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira. Sheria hii inaipa Bodi ya Wakurugenzi mamlaka ya kipekee ya kupata leseni za utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika maeneo yake ya mamlaka. Aidha, sheria hiyo inalenga kushughulikia udhaifu na changamoto zinazoikabili sekta ya maji nchini.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), ikiwa ni miongoni mwa mamlaka za maji mijini, ni taasisi huru ya kisheria iliyoanzishwa tarehe 1 Julai 1998 chini ya Sheria ya Maji, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 1997, na baadaye kufutwa na kubadilishwa na Sheria ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009. Sheria hiyo imeipa MUWASA jukumu la kusambaza maji safi na salama pamoja na kutoa huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma kwa gharama nafuu na ubora unaokubalika, kwa kuzingatia viwango vya huduma na miongozo inayotolewa na Wizara ya Maji na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Dira
Kuwa mamlaka inayoongoza kwa kutoa huduma bora za maji safi na usafi wa mazingira kwa wateja nchini Tanzania.
Dhima
Kutoa huduma za uhakika za maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira ili kusaidia ustawi wa jamii na shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Mara.

