Watendaji sekta ya m...
Watendaji sekta ya maji watakiwa kuacha alama
22 Jul, 2026
Watendaji sekta ya maji watakiwa kuacha alama

Watendaji wa Sekta ya Maji wametakiwa kuacha alama katika utendaji wao kwa kuzingatia matokeo, uwajibikaji na ubora wa huduma za maji kwa kila mwananchi.

Wito huo umetolewa wakati Serikali ikiimarisha utaratibu wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora unaolenga maslahi ya wananchi.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.), ametoa wito huo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya utendaji kati ya Wizara ya Maji, Bodi za Maji za Mabonde na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini.

Waziri Aweso amesema mikataba iliyotiwa saini ni ahadi ya uwajibikaji na ufanisi kwa watendaji katika kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha malengo na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amewataka watendaji wa taasisi zote za Sekta ya Maji kutimiza malengo waliyojiwekea kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma.

Amebainisha kuwa rasilimali za maji ni suala la usalama wa taifa, na kuitaka Bodi ya Taifa ya Maji pamoja na Bodi za Maji za Mabonde kusimamia, kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya sasa na ya baadaye.

“Bodi za Maji za Mabonde zinatakiwa kuwa na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa takwimu sahihi za rasilimali za maji, kwani ndiyo msingi wa kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya sekta na taifa kwa ujumla,” amesema Waziri Aweso.

Aidha, amezitaka Mamlaka za Maji kuboresha huduma zake.

Amesisitiza kuwa mwaka wa fedha 2026/27 ni mwaka wa kuongeza kasi kiutendaji kupitia uboreshaji wa mifumo ya utawala bora, upunguzaji wa malalamiko ya wateja, uongezaji wa uzalishaji wa maji, udhibiti wa upotevu wa maji na uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema sekta ya maji inaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa vipimo vya utendaji kazi vitatumika kama kigezo cha kupima uwezo na ufanisi wa watendaji kuendelea kubaki katika nafasi zao.

slot gacor